Monday, 17 November 2014

VAMPIRE: Suarez kupoteza Pauni 3 milioni aking’ata Barcelona

 
Suarez ambaye ameanza taratibu maisha yake ya soka Barcelona anachukua dau la pauni 10 milioni kwa mwaka, lakini inadaiwa kuwa atakatwa dau la pauni 3 milioni kama akimng’ata mchezaji wa timu pinzani. 

LUIS Suarez itabidi awe mpole tu. Imegundulika kuwa kama akifanya tena ujinga wake wa kung’ata mtu pale Nou Camp basi atalambwa dau kubwa la mshahara wake wa mwaka, hii ni kwa mujibu wa mkataba wake na Barcelona.
Suarez ambaye ameanza taratibu maisha yake ya soka Barcelona anachukua dau la pauni 10 milioni kwa mwaka, lakini inadaiwa kuwa atakatwa dau la pauni 3 milioni kama akimng’ata mchezaji wa timu pinzani.
Nyota huyo wa kimataifa wa Uruguay tayari amewang’ata wachezaji watatu katika maisha yake ya soka akichezea klabu za Ajax, Liverpool na timu yake ya taifa ya Uruguay.
Novemba 20, 2010 alimng’ata mchezaji wa PSV, Otman Bakkal katika pambano la Ligi Kuu ya Uholanzi lililomalizika kwa suluhu ya bila kufungana. Klabu yake ya Ajax ilimsimamisha mechi mbili na kumtoza faini.
Kama vile haitoshi, April mwaka jana alimng’ata mlinzi wa Chelsea, Branislav Ivanovic katika pambano la Ligi Kuu ya England uwanja wa Anfield. FA ilimfungia mechi 10 za Ligi Kuu ya englad.
June mwaka huu alimalizia Hat trick yake ya kung’ata wakati alipomng’ata mlinzi wa timu ya taifa ya Italia, Giorgio Chielini katika pambano la kombe la dunia nchini Brazil. Alifungiwa kucheza soka kwa miezi minne huku akifungiwa mechi kumi za timu yake ya taifa ya Uruguay.
Hata hivyo, baada ya uhamisho huo, staa huyo alikamilisha uhamisho wa pauni 75 milioni kwenda Nou Camp kutoka Anfield huku akiingia mkataba wa miaka mitano ambayo unamfanya alipwe mshahara wa pauni 200,000 kwa wiki. Mshahara huo unamfanya awe mchezaji wa nne kwa kulipwa zaidi katika klabu ya Barcelona nyuma ya Lionel Messi, Neymar na Andres Iniesta, lakini huenda ukashuka maradufu kama akiendeleza tabia zake za Ajax na Liverpool.
Mkataba wa Barcelona kwa Suarez ni mkali na utamuona mchezaji huyo akipoteza kiasi cha asilimia 15 hadi 30 ya mshahara kama akirudia kung’ata wachezaji wa timu pinzani.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa mabosi wa Barcelona kwa kiasi kikubwa walishukuru kitendo cha Suarez kumng’ata Chiellini  kwa sababu kwa kiasi kikubwa kiliharakisha mazungumzo kati ya timu yao na Anfield.
Kitendo hicho kilishusha thamani ya Suarez kwa kiasi kikubwa na ni timu chache ambazo ziliamua kufukuzia saini yake mara baada ya kung;ata nchini Brazil.
Kuhakikisha kwamba tukio hilo halitokei tena, hivi karibuni nyota huyo amekiri kwamba kwa sasa anapata msaada wa matibabu ya kisaikolojia kuhakikisha kwamba hawezi kufanya tena kitendo hicho katika siku za karibuni.

No comments:

Post a Comment